MACHANGU AZIOMBA MAHAKAMA KUONGEZA ADHABU KWA WAHALIFU WA UBAKAJI NA ULAWITI
ALIYEKUWA MBUNGE WA VITI MAALUM MKOA WA KILIMANJARO, KUPITIA CHAMA CHA MAPINDUZI BETTY MACHANGU
MOSHI.
MAHAKAMA nchini zimeombwa kutoa adhabu
kali kwa wanaume ambao wamekuwa wakipatikana na hatia ya ubakaji na ulawi kwa
watoto ili kuwa fundisho na kusaidia kupunguza matatizo hayo ambayo yameonekana
kushamiri.
Kauli hiyo ilitolewa na aliyekuwa
Mbunge wa viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Betty Machangu (CCM) alipozungumza
na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa, wanaume wanaofanya vitendo hivyo
wamekuwa wakichangia kwa asilimia kubwa kuwaharibia maisha watoto hao.
Machangu alisema kuwa, kutokana na
kumuharibia mtoto maisha mwanaume huyo anapaswa kupewa adhabu kali ambayo
itakuwa fundisho kwa jamii nzima kutambua kuwa kufanya hivyo ni kosa kinyume na
sheria na adhabu yake huwa ni kali.
“Vitendo hivi vimekuwa vikikuwa kwa
kasi sana kutokana na mahakama kutoa adhabu ndogo kwa wahusika wanaofanya hivi
vitendo hivyo niiombe mahakama iangalie upya adhabu ambazo wamekuwa wakizitoa
kwa hawa wahusika na waongeze” alisema Machangu.
Mbunge huyo alitoa mfano hukumu
iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita katika mahakama ya hakimu mkazi mkoani
Tabora, ambapo ilimtia hatiani Sadick Masunzu (47), kwa kosa la kumbaka binti
yake mwenye umri wa miaka 16 na kumpatia ujauzito ambapo alihukumiwa kutumikia
kifungo cha miaka 4.
Alisema kuwa, adhabu hiyo aliyopewa
Masunzu ni ndogo ukilinganisha na kosa alilolifanya ambapo amemuharibia binti yake maisha kwa kumbebesha mimba.
“Inasikitisha sana kuona mtu ametiwa
hatiani kwa kosa la kubaka alafu anahukumiwa kifungo cha miaka minne hii ni
aibu sana tunawaomba mahakimu muangalie upya hizi adhabu vinginevyo vitendo
hivi vya ubakaji na ulawiti vitaendelea kutokana na adhabu kuwa ya kawaida tu”
alisema Machangu.
Aidha Machangu aliiomba jamii kuwa
mstari wa mbele katika kuwafichua wanaume ambao wamekuwa wakiwafanyia watoto wa
kike unyama huo ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki na kukomesha vitendo
hivyo.
Mwisho……………….


Maoni
Chapisha Maoni