SERIKALI IMEJIPANGA KUMALIZA KERO ZA WALIMU…


KATIBU TAWALA WA MKOA WA KILIMANJARO, MHANDISI AISHA AMOUR (wa pili kulia),AKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA WAJUMBE NA VIONGOZI WA CHAMA CHA WALIMU MKOA WA KILIMANJARO (wa kwanza kushoto) MWENYEKITI WA CWT MKOA, OMARY MCHOMVU AKIFUATIWA NA KATIBU WA CWT MKOA, DIGNA NYAKI NA WA KWANZA KULIA NI MJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI TAIFA, SALMA KIMARO. 
 
MOSHI.

KATIBU Tawala mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Aisha Amour amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu zinapatiwa ufumbuzi huku akishitushwa na tatizo la walimu mkoa hapa kucheleweshewa mafao yao ya kustaafu.

Mhandisi Amour alitoa kauli hiyo katika baraza la dharura la chama cha Walimu (CWT), mkoa wa Kilimanjaro ambapo alisema kuwa, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa walimu katika kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Serikali inatambua changamoto mbalimbali ambazo nyinyi walimu mmekuwa mkikabiliana nazo ikiwamo madeni yenu lakini zipo juhudi mbalimbali ambazo zimefanywa na serikali ili kuhakikisha kuwa changamoto zote zinapatiwa ufumbuzi hivyo msife moyo tambueni serikali ipo pamoja na nyie” alisema Mhandisi Amour.

Katibu Tawala huyo wa mkoa alisikitishwa na changamoto ya walimu katika mkoa wa Kilimanjaro kucheleweshewa mafao yao ya wastaafu na kudai kuwa Serikali ilishakataza ucheleweshaji wa mafao kwa watumishi wanaostaafu hali iliyompelekea kukitaka chama cha walimu mkoa kumwandikia orodha ya majina ya walimu waliocheleweshewa mafao ili aweze kulishughulikia.

Akizungumzia swala la Walimu wa Sekondari kuhamishwa kwenda kufundisha shule za msingi alisema kuwa, yapo malalamiko mbalimbali yaliyotolewa na walimu katika zoezi hilo ambapo wapo baadhi ya Watumishi wa halmashauri mkoa Kilimanjaro wamekuwa wakitumia kigezo cha kuwakomoa walimu kutokana na chuki binafsi.

Alisema kuwa kwa sasa ameunda tume maalum ambayo imeanza kupita kila halmashauri ili kujua jinsi zoezi la kuwahamisha walimu kutoka sekondari kwenda kufundisha shule za msingi jinsi lilivyofuata kanuni na vigezo vilivyowekwa.

Aidha Mhandisi Amour alisema kuwa, Walimu wengi wamekuwa wakiilaumu Serikali kutokana na baadhi ya Watendaji wa halmashauri kutotimiza wajibu wao na kudai kuwa hata mvumilia Mtendaji yeyote wa Serikali katika mkoa huo atakayekiuka matakwa ya Serikali na kupelekea kuingia katika lawama.

Akizungumzia tatizo la baadhi ya halmashauri kuwaondoa walimu katika malipo alisema kuwa limekuwa tatizo kubwa hali ambayo imemlazi kuunda timu maalum ambayo imekuwa ikipita kila halmashauri kuchukua majina ya walimu walioondolewa pamoja na sababu za kuwaondoa ili kujua nini tatizo na kuomba kupewa muda ili aweze kulitolea ufafanuzi baada ya kupata majinu ya tume hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha walimu mkoa wa Kilimanjaro, Omary Mchomvu alisema kuwa, hakuna watu wenye nidhamu kama walimu kama wakitendewa haki zao za msingi na kutumia nafasi hiyo kuiomba serikali kutimiza matakwa ya walimu.

Mchomvu alisema kuwa, walimu katika mkoa wa Kilimanjaro amekuwa wakiwajibika kwa vitendo na hiyo imejidhihirisha baada ya mkoa kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne na kudia kuwa chama chao kimejipanga kuhakikisha mkoa unaendelea kushika nafasi hiyo.

Awali akisoma risala ya Walimu kwa Katibu Tawala, Katibu wa CWT mkoa wa Kilimanjaro, Digna Nyaki alisema kuwa, walimu wa mkoa wa Kilimanjaro wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Nyaki alisema kuwa miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na walimu waliohamishwa kutoka shule za sekondari kwenda shule za msingi mkoani hapa wamehamishwa bila kulipwa gharama zao za uhamisho kinyume na kauli ya Rais Dk. John Pombe Magufuli aliyotoa Desemba mwaka jana mjini Dodoma.

Dk. Magufuli akifungua mkutano mkuu wa chama cha walimu Taifa Dodoma 

KATIBU WA CWT MKOA WA KILIMANJARO, DIGNA NYAKI.
 
alisema kuwa, mwalimu asihamishwe bila mwajiri kuwa na fedha ya kumlipa lakini katika hali ya kushangaza waajiri wamekuwa wakifanya hivyo.

Alisema kuwa, changamoto nyingine ni kutolipwa kwa deni lao shilingi Bilioni 1.131 ambapo deni hilo ni kwa walimu wa mkoa wa Kilimanjaro pekee ambayo sio ya mishahara na yalishahakikiwa na serikali kwa kushirikiana na chama cha walimu.

Mwisho….
 WAJUMBE WA BARAZA LA CHAMA CHA WALIMU MKOA WA KILIMANJARO WAKIFUATILIA KWA MAKINI HOTUBA YA MGENI RASMI KATIKA BARAZA HILO AMBAYE NI KATIBU TAWALA WA MKOA WA KILIMANJARO, MHANDISI AISHA AMOUR (HAYUPO PICHANI)


 MJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI TAIFA, SALMA KIMARO AKIMPA ZAWADI ILIYOANDALIWA NA WALIMU MGENI RASMI KATIKA BARAZA HILO AMBAYE NI KATIBU TAWALA WA MKOA WA KILIMANJARO, MHANDISI AISHA AMOUR.



KATIBU WA CHAMA CHA WALIMU MKOA WA KILIMANJARO, DIGNA NYAKI AKIFURAHIA JAMBO MARA BAADA YA KUHITIMISHA BARAZA HILO JANA.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Mama ajifungua mapacha wenye baba tofauti

MHUDUMU AANGUKA KUTOKA KWENYE NDEGE UGANDA

Ufahamu ugonjwa wa Ngiri ( Hernia) kiundani zaidi