TRA YAINGIZA MILIONI 368.77 KUTOKANA NA BIDHAA ZA MAGENDO ..
MOSHI.
MAMLAKA ya Mapato nchini TRA, mkoa wa
Kilimanjaro imekusanya kiasi cha shilingi milioni 368.77 kama kodi na faini za
bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kinyume na sheria katika kipindi cha
Julai mwaka jana hadi Februari mwaka huu.
Hayo yalibainishwa na Meneja msaidi
wa mamalaka hiyo mkoa wa Kilimanjaro anayeshughulikia maswala ya forodha,
Godfrey Kitundu wakati alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na
kudai kuwa, wapo baadhi ya Wananchi ambao sio waaminifu wamekuwa wakiingiza
nchini bidhaa za magendo.
Kitundu alisema kuwa, Wafanyabiashara
hao wamekuwa wakitumia njia zisizo rasmi (njia za panya), kupitisha bidhaa hizo
ambapo katika mkoa wa Kilimanjaro zipo njia zisizo rasmi zipatazo zaidi ya 300.
Alisema kuwa, mkoa wa Kilimanjaro
unapakana na nchi jirani ya Kenya ambapo unanjia halali tatu zilizohidhinishwa
na Serikali ambazo ni Holili, Tarakea na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA), ambazo ndizo njia zilizopendekezwa na Serikali kupitisha mizigo
mbalimbali.
Meneja huyo alibainisha kuwa, bidhaa
ambazo zimekuwa zikiingizwa nchini kwa njia za magendo ni Sukari inayozalishwa
kutoka nchini Brazili na Msumbiji ambapo tokea mwezi Desemba mwaka jana paka
sasa jumla ya Tani 41 sawa na kilogramu 4100, imeshakamatwa ambapo paka sasa
wanaishikilia.
Aliendelea kudai kuwa, bidhaa
nyingine ni mafuta ya taa ambapo kuanzia mwezi Julai mwaka jana paka sasa jumla
ya lita 27000 zilikamatwa, chumvi zikiwa katoni 2000 na bidhaa ndogo ndogo kama
pipi zikiwa katoni 397.
“Wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao
sio waaminifu wamekuwa wakiingiza bidhaa mbalimbali nchini kwa kutumia njia
zisizo rasmi huku wakitambua kuwa kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi wa nchi na
kuvizorotesha viwanda vya ndani” alisema Kitundu.
Meneja huyo aliendelea kudai kuwa, bidhaa
hizo zimekuwa zikiingizwa nchini kwa kutumia usafiri wa pikipiki na magari
ambapo toka mwezi Julai mwaka jana paka
sasa jumla ya pikipiki 52 na magari 17
yalikamatwa yakiingiza bidhaa za magendo nchini.
Kwa mujibu wa sheria za nchi chombo
chochote cha usafiri kikikamatwa kikiwa kinasafirisha bidhaa za magendo adhabu
yake ni kukitaifisha.
Aidha Meneja huyo alisema kuwa, TRA
wamekuwa wakishirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama wakiwamo
jeshi la Polisi na Wananchi wenye nia njema na Taifa katika kuwabaini na
kuwakamata wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiingiza bidhaa hizo za magendo
nchini.
Katika hatua nyingine alisema kuwa,
kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya magari ya kufanyia operesheni katika
eneo lote la mpaka, huku pia wamekuwa wakiendelea kuwaelimisha Wananchi kuacha
tabia ya kupita njia za panya na badala yake wapiti njia rasmi na kulipa kodi
kulingana na bidhaa alizonazo.
Mwisho
Maoni
Chapisha Maoni