VIONGOZI WA CHAMA CHA MAPINDUZI NA JUMUIYA ZAKE WATAKIWA KUACHA KULALAMIKA NA BADALA YAKE WASHIRIKIANE KUTATUA KERO ZA WANANCHI…..
MOSHI.
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya
Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani Kilimanjaro Daudi Mrindoko amewataka viongozi
wa chama na jumuiya kuanzia ngazi ya kata kuacha tabia ya kulalamika na badala
yake wajitoe kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi matatizo yanayowakabili Wananchi ili
waendelee kukiamini chama.
Mrindoko alitoa kauli hiyo jana
wakati wa maadhimisho ya wiki la juma la wazazi wilaya ya Moshi mjini ambapo
walipanda miti zaidi ya 200 katika shule ya Sekondari ya Kibo inayomilikiwa na
Jumuiya hiyo.
MWENYEKITI WA JUMUIYA YA WAZAZI YA CCM MKOA WA KILIMANJARO, DAUDI MRINDOKO.
Alisema kuwa, wapo baadhi ya viongozi
wamekuwa na tabia ya kujenga lawama kwa viongozi wa juu bila kutambua kuwa hata
wao wanajukumu la kuhakikisha wanashirikiana kutafuta ufumbuzi wa matatizo
yanayowakabili Wananchi.
“Wapo baadhi ya viongozi wamekuwa
wakiwabebesha mizigo na lawama viongozi wa juu wakati misingi ya chama chetu ni
kushirikiana viongozi wote kuhakikisha tunawatumikia Wananchi na kuwatatulia
matatizo yao ili waendelee kukiamini na kukipenda chama chetu” alisema
Mrindoko.
Akizungumzia swala la maadili kwa vijana
Mwenyekiti huyo alisema kuwa, swala la maadili lipo chini ya Wazazi na kuwataka
wanachama wa Jumuiya hiyo kuwa mfano bora katika kusimamia maadili na malezi
ili kuwafanya jamii kuiga mfano bora toka jumuiya hiyo.
Aidha Mrindoko alisema kuwa, Jumuiya
hiyo ambayo ni kongwe katika mkoa wa Kilimanjaro ilikuwa ikimiliki vitega
uchumi mbalimbali zikiwamo shule lakini wapo baadhi ya viongozi wenye uchu
binafsi waliuza baadhi ya shule na kudai kuwa katika kipindi chake cha uongozi
hatakubali kuona mali za jumuiya zikiuzwa na badala yake atazisimamia kwa
ukaribu ili kuona zinanufaisha jumuiya na chama.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti
huyo alisema kuwa, zipo baadhi ya shule za Jumuiya ambazo zimefungwa kutokana
na kukosa Wanafunzi na kuwataka Wanachama wa ccm pamoja na wawekezaji wanaotaka
kuwekeza katika Elimu kufika katika ofisi za Jumuiya ya Wazazi mkoa ili kuona
uwezo wa kuendeleza shule hizo zilizofungwa.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza kuu
la Wazazi Taifa, Alhaji Mollel aliwataka viongozi wa chama na Jumuiya
kuimarisha chama kwa kuongeza wanachama ili pindi miaka mitano ya uongozi wao
itakapokwisha wajivunie kwa kuacha historia nzuri.
Mollel alitumia nafasi hiyo kuwataka
viongozi wa dini kuacha kuponda maendeleo yanayofanywa na viongozi wa Serikali
na kubaki katika misingi yao ya Biblia na Misaafu, na kuachana na kuhubiri
siasa katika Nyumba za ibada.
“Viongozi wa dini mnapaswa kutenga
maswala ya dini na kisiasa kwani kila jambo linasehemu yake na mnapaswa
kutambua kuwa katika nyumba za Ibada wapo waumini wa vyama mbalimbali hivyo
mnaweza kusababisha mpasuko ndani ya nyumba za ibada” alisema Mollel.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi
wilaya ya Moshi mjini, Juma Mohamed alisema kuwa, lengo la Jumuiya hiyo katika
wilaya ya Moshi mjini ni kuhakikisha inaboresha Elimu hususani katika shule ya
Sekondari ya Kibo ambayo inamilikiwa na Jumuiya hiyo pamoja na kusimamia
maadili.
Mohamed alisema kuwa, kipindi cha
nyuma Jumuiya hiyo imedharaulika machoni pa watu kwa kushindwa kusimamia
maadili na kudai kuwa kwa sasa wamejipanga kurudisha heshima na kudai kuwa
hawatamvumilia mtu atakayekuwa chanzo cha kukwamisha malengo yao.
Mwisho…..




































Maoni
Chapisha Maoni