ZIARA YA MWENYEKITI WA UVCCM MKOA WA KILIMANJARO WILAYANI ROMBO YAIBUA MADUDU…..WATUMISHI WA HALMASHAURI WADAIWA KUFUJA FEDHA ZA VIJANA WENYEWE WASHINDWA KUJITETEA…





ROMBO.

ZIARA ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), mkoa wa Kilimanjaro Ivan Moshi, imeibua madudu katika halmashauri ya wilaya Rombo baada ya kubainika Watumishi wa halmashauri hiyo pamoja na Madiwani wake wamekuwa wakikopeshana fedha zinazotengwa kwa ajili ya vikundi vya vijana.

Mwenyekiti huyo aliyefanya ziara hiyo jana na kukutana na Wajumbe wa Baraza kuu la vijana wilaya, ambapo wajumbe hao waliibua mambo mazito ambayo yamekuwa yakifanywa na Watumishi wa halmashauri hiyo huku.

Katika hali ya kushangaza  Afisa Maendeleo Vijana wa Halmashauri hiyo, Florentine Langu aliyetakiwa kuwepo katika kikao hicho kwa niaba ya Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, ili aweze kujibu tuhuma hizo alifika wakati wanahitimisha kikao hicho kutokana na kile alichodai kuwa alizuiwa na Kaimu Mkuregenzi wa Halmashauri ya Rombo, ambaye ni Mhandisi wa Maji aliyetambulika kwa jina moja la Msangi.

Wajumbe hao wa baraza walisema kuwa, Watumishi hao wa Halmashauri pamoja na Madiwani wamekuwa wakiunda vikundi vyao binafsi ni kujikopesha fedha hizo ambazo ni asilimia tano ya mapato ya ndani huku vikundiambavyo vimekuwa vikiundwa na vijana vikikosa fedha hizo kutokana na kile wanachoelezwa kuwa hawana sifa ya kukopa.

Afisa Maendeleo huyo wa Vijana, Florentine Langu alipotakiwa kujibu tuhuma hizo zilizoelezwa na wajumbe wa Baraza hilo, alishindwa kukanusha au kukubali na badala yake alitoa orodha ya vikundi 27 ambavyo vimepatiwa mkopo na Halmashauri.

Kutoa kwa orodha hiyo kuliibua kelele na maswali mengi kutokana na orodha ya vikundi hivyo kuwa ni hewa ambapo havijulikana huku vikundi vikinge vikitajwa kunufaika na mkopo ili hali havijapatiwa fedha yoyote.

Hali hiyo ya sintofahamu ilimlazimu Mwenyekiti wa mkoa kuahidi kulifikisha swala hilo katika ngazi za juu ili kuhakikisha kuwa Vijana wa Rombo wanapata haki yao ya msingi inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi.

Moshi alisema kuwa, Umoja wa Vijana mkoa wa Kilimanjaro umejipanga kuhakikisha wanatetea maslahi ya vijana wa mkoa huo huku akiwataka Viongozi kuhakikisha vijana wananufaika na fursa zinazotolewa na Serikali.

“Huu ni wakati ambao viongozi tunapaswa kuacha tabia ya kuongoza kimazoea na badala yake tutafute mbinu za kuwainua vijana kimaendeleo na kutetea maslahi yao binafsi na pindi unapoona mtumishi wa Serikali anataka kuchezea maslahi ya vijana usimfumbie macho mripoti kwetu ili na sisi tumfikishe panapohusika” alisema Moshi.

Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM mkoa wa Kilimanjaro, Abdulrahimu Hamad alisema kuwa, vijana wamekuwa wakitumika kipindi cha uchaguzi na pindi viongozi wanapopatika wamekuwa wakiwasahau na kuwataka vijana kutokubali kufanywa tambara la dekio.

Hamad alisema kuwa, viongozi wote bila kujali itikadi ya vyama wanawajibu wa kuyasimamia maendeleo ya vijana na sio kuwatumia kwa maslahi yao binafsi.

“Vijana tumekuwa tukitumika kufanya maandamano na kuvuruga amani ya nchi yetu wakati katika maandamano hayo pindi mnapata matatizo viongozi hao wanaowaeleza muandamane wamekuwa hawawasaidii kwa chochote ifike mahali na sisi tusikubali kutumika ovyo kwa maslahi ya mtu mwingine” alisema.

Mwisho…………..

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ufahamu ugonjwa wa Ngiri ( Hernia) kiundani zaidi

Mama ajifungua mapacha wenye baba tofauti

UVCCM SIHA YAZINDUA KAMPENI YA KUGAWA TAULO ZA KIKE KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI