WAHITIMU WA KIDATO CHA SITA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA SIASA CHAFU

                                                                    MOSHI.

MGENI RASMI KATIKA MAHAFALI YA KIDATO CHA SITA KATIKA SHULE YA SEKONDARI YA MAWENZI, MWENYEKITI WA JUMUIYA YA WAZAZI MKOA WA KILIMANJARO, DAUDI MRINDOKO (katikati), AKIWA NA MKUU WA SHULE YA SEKONDARI YA MAWENZI  CHRISTINE SHIRIMA (kushoto), NA KULIA NI MWENYEKITI WA BODI YA SHULE HIYO PROFESA CHAMBO.


WAHITIMU wa kidato cha sita mwaka 2018, nchini wameshauriwa kuacha tabia ya kufanya siasa chafu pamoja na biashara haramu ya madawa ya kulevya na badala yake watumie elimu waliyoipata katika kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM mkoa wa Kilimanjaro, Daudi Mrindoko katika mahafali ya 26 ya kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Mawenzi iliyopo manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo jumla ya wanafunzi wa kike 229 wanahitimu.

Mrindoko alisema kuwa, wapo baadhi ya watanzania wamekuwa wakieneza siasa chafu (maji taka), huku wakitambua kuwa zinaweza kuvuruga amani ya nchi iliyodumu kwa muda mrefu na kusababisha machafuko.

“Natambua kuwa mnahitimu elimu yenu ya kidato cha sita na kurejea majumbani kusubiria matokeo niwasihi kuhakikisha msije kujiingiza katika siasa chafu na kupelekea kupoteza amani yetu bali mtumie elimu mliyoipataka katika kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo” alisema Mrindoko.

WAHITIMU WA KIDATO CHA SITA KATIKA SHULE YA SEKONDARI YA MAWENZI.

Mwenyekiti huyo pia aliwahusia wanafunzi hao, kuzingatia maadili wawapo majumbani na kuepuka kushawishiwa na watu wasio na maadili na kupelekea kuharibu maisha yao ya badae.

Awali akisoma risala ya shule kwa mgeni rasmi, mkuu wa shule ya Mawenzi, Christine Shirima alisema kuwa, shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo upungufu mkubwa wa nyumba za watumishi kwani shule hiyo inanyumba saba huku hali ya idadi ya watumishi ikiwa ni 82.

Shirima alisema kuwa, changamoto nyingine ni uhaba wa vitabu katika masomo ya uchumi na hisabati, bwalo la chakula ni dogo  hivyo inawalazimu wanafunzi kula chakula chini ya miti, madarasani na mabwenini.

“Changamoto nyingine inayotukabili ni kutokukamilika kwa uzio wa shule kutokana na uhaba wa fedha, lakini pia shule haina muuguzi (nesi) na hali hii inasababisha wanafunzi kupoteza muda mwingi kufuatilia matibabu kwani hata wale ambao wangeweza kupata huduma ya kwanza na kuendelea na masomo wanashinda hospitali siku nzima kusubiria matibabu” alisema Shirima.

Akizungumzia swala la ufauli, Mkuu huyo wa shule alisema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita ambapo mwaka 2014 ufauli kwa daraja la kwanza hadi la tatu ulikuwa kwa asilimia 95.6. huku mwaka 2015 ukiwa kwa asilimia 97.1, na mwaka 2016 pamoja na 2017 ufaulu ulikuwa kwa asilimia 100.

Wakisoma risali ya wahitimu  kwa mgeni rasmi, walisema kuwa miongongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni baadhi ya miundombinu ya shule ni mibovu ikiwemo mifumo ya vyoo ndani ya mabweni na kupelekea vyoo vingine kutotumika hali ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu na msongamano katika bafu na vyoo vya nje.

Shule hiyo imekuwa ikipokea michepua ya HGL, HGK, HKL na HGE kwa wanafunzi wa kike pekee ambapo ni miongoni mwa shule ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kitaifa.










                                                                               
                                                                                                                                                        MWISHO.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ufahamu ugonjwa wa Ngiri ( Hernia) kiundani zaidi

Mama ajifungua mapacha wenye baba tofauti

UVCCM SIHA YAZINDUA KAMPENI YA KUGAWA TAULO ZA KIKE KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI