MABIHYA AWAKABIDHI SWALA LA ULINZI WA WANANCHI WA KATA YA MAWENZI NA MAKANYA KWA UVCCM

Mishima.


KATIBU WA CHAMA CHA MAPINDUZI MKOA WA KILIMANJARO, JONATHAN MABIHYA WA KATI KATI AKIWA KATIKA KIKAO CHA BARAZA KUU LA UMOJA WA VIJANA MKOA WA KILIMANJARO JANA, KUSHOTO NI MWENYEKITI WA UVCCM MKOA WA KILIMANJARO, IVAN MOSHI NA KULIA NI KATIBU WA UVCCM MKOA ABDULRAHIMU HAMAD.
VIJANA wa chama cha mapinduzi (UVCCM), mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kuhakikisha wanalinda wananchi wa kata ya Mawenzi iliyopo manispaa ya Moshi pamoja na Makanya wilayani Same wasitishwe na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani.

Alidai kuwa kata hizo mbili zinazotarajia kupiga kura Agosti 12 mwaka huu kumpata Diwani atakayewaongoza kipindi kilichobakia wamekuwa wakitishwa na baadhi ya viongozi wa vyama.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya katika ufunguzi wa baraza la UVCCM mkoa wa Kilimanjaro ambapo alisema kuwa, vijana wa chama cha mapinduzi wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi na wanachama wa ccm wanatimiza maamuzi yao ya kikatiba.

"Wapo baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ambao baada ya kuona dalili za kushindwa wameanza kupita kwa wananchi na kuwapa maneno ya vitisho ili wasijitokeze kupiga kura sasa nyie vijana wa ccm mnajukumu kubwa la kuhakikisha mnawalinda wananchi" alisema Mabihya.



WAJUMBE WA BARAZA KUU LA UMOJA WA VIJANA (UVCCM) MKOA WA KILIMANJARO WAKIENDELEA NA KIKAO CHA BARAZA JANA.

Mabihya alitumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa Uvccm kuanzia ngazi ya tawi hadi mkoa kuwa wasemaji na wafuatiliaji wa matatizo ya vijana na sio kugeuka kuwa walalamikaji.

Alisema kuwa, zipo baadhi ya wilaya ambazo makatibu wa umoja huo wamekuwa hawana imani na Wenyeviti wake waliochaguliwa na kuwataka makatibu hao kuondoa tofauti hizo kwa manufaa mapana ya chama.

Akizungumzia swala la Uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa mwakani pamoja na ule mkuu mwaka 2020, amewataka vijana kutotumika vibaya na kuwa sehemu ya makundi ndani ya chama badala yake wanapaswa kuwaachia wanaccm wenyewe wamchague kiongozi wamtakaye.

"Vijana mmekuwa mkitumika vibaya katika kutengeneza makundi ndani ya chama niwaonye viongozi wa vijana msikubali kutumika na kiongozi tutakayembaini hatutasita kumchukulia hatua" alisema Mabihya.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi amewataka vijana wa chama cha mapinduzi kufanya kazi kwa kushirikiana kwa maslahi mapana ya Taifa na chama kwa ujumla.

Moshi aliwataka viongozi wa umoja huo wilaya kuhakikisha wanatetea maslahi ya vijana waliowaamini na kuwachagua pamoja na kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili.

Naye Katibu wa umoja huo mkoa,  Abdulrahimu Hamad alisema kuwa, jukumu kubwa la vijana ndani ya CCM ni kuhakikisha chama hicho kinashinda katika chaguzi kuu na serikali za mitaa ili kuendelea kushika dola.

Alisema UVCCM mkoa wa Kilimanjaro kwa sasa wamejidhatiti kuufuta upinzani katika mkoa huo na kudai kuwa wamejipanga vyema kuhakikisha lengo hilo linatimia ifikapo mwaka 2020.



Mwisho.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ufahamu ugonjwa wa Ngiri ( Hernia) kiundani zaidi

Mama ajifungua mapacha wenye baba tofauti

UVCCM SIHA YAZINDUA KAMPENI YA KUGAWA TAULO ZA KIKE KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI