UVCCM SIHA YAZINDUA KAMPENI YA KUGAWA TAULO ZA KIKE KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
SIHA
![]() |
| MWENYEKITI WA WA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI (UVCCM) WILAYA YA SIHA WILSON MUSHI |
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wameanza kampeni maalum ya kugawa taulo za kike katika shule za msingi na sekondari wilayani humo yenye lengo la kuhakikisha wananfunzi wa kike waliofikia katika umri wa kuvunja ungo wanashiriki masomo katika kipindi chote wanapofikia katika siku zao za hedhi.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa jana na Mwenyekiti wa Uvccm wilaya ya Siha, Wilson Mushi alisema kuwa, katika utafiti uliofanywa mwaka 2014 wilayani humo kulibainika kuwa asilimia 82 ya wanafunzi wa kike wamekuwa wakikosa masomo pindi wanapokuwa katika siku zao za hedhi.
Mushi alisema kuwa, hali hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma ufaulu wa watoto wa kike katika mitihani yao ya ndani pamoja na ile ya kitaifa hali ambayo imesukuma jumuiya hiyo kuamua kuanzisha kampeni hiyo maalum ya kuwasaidia watoto hao.
"Wapo watoto ambao hutoka katika familia za hali ya chini ambapo wazazi wamekuwa wakishindwa kuwanunulia watoto taulu za kike ili waweze kujisitiri katika kipindi cha hedhi hali ambayo imekuwa ikipelekea watoto kushindwa kuhudhuria shule katika kipindi hicho na kukosa masomo" alisema Mushi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa, kwa kuanza kampeni hiyo umoja huo wa vijana umepanga kugawa taulo hizo za kike katika shule za msingi na sekondari zipatazo 20 zilizopo katika kata 8 za wilaya ya Siha na badae wanatarajia kumalizia katika shule zilizopo katika kata 9 ili kuhitimisha kata 17 za wilaya ya Siha.
Aidha Mwenyekiti huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka Walimu pamoja na Wazazi kutoa elimu ya jinsia pamoja na hedhi kwa watoto wa kike bila kumumunya maneno ili waweze kuwa na uelewa mpana juu ya hali hiyo na kutambua nini wafanye pindi wanapotokewa na hali hiyo.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM wilaya ya Siha, Agnes Msuya alisema kuwa, kampeni hiyo iliyoanzisha na umoja wa vijana itasaidia kuboresha maisha ya watoto wa kike kifikra na kiakili kwa kutambua mabadili ya miili yao pamoja na kwasaidia kupata taulo maalum za kujisitiri pindi wanapokuwa katika siku zao.
Agnes alisema kuwa, wapo baadhi ya watoto wa kike hususani wanaoishi vijijini wamekuwa hawana elimu ya kutosha juu ya mabadiliko hayo na hii inatokana na walimu pamoja na wazazi kutowaeleza ukweli juu ya swala zima la hedhi na kuwataka kubadilika ili kuwafanya watoto hao kuwa huru pindi wanapofikwa na hali hiyo.
Aliongeza kuwa zipo baadhi ya shule ambazo hazijatenga chumba maalum kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujisitiri pindi wanapokuwa katika siku zao na kudai kuwa kampeni hiyo itaenda sambamba na kuhakikisha kila shule inatenga chumba cha watoto wa kike kujisitiri.
Naye Katibu wa Uvccm wilaya ya Siha, David Mollel alisema kuwa, umoja huo wa vijana unawajibu wa kulea vijana kuja kuwa viongozi wa badae na kwa kutambua hilo wameamua kupambana na changamoto inayowakabili watoto wa kike wilayani Siha.
Mollel alisema kuwa, kampeni hiyo utakuwa ya mwendelezo katika wilaya ya Siha na kudai kuwa, ni moja ya mikakati ya mpango kazi waliojiwekea mwaka 2018-19 katika kuhakikisha wanaondoa changamoto za vijana.
Mwisho
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine


Maoni
Chapisha Maoni