WAZIRI KAIRUKI AWAFUNDA WANANCHI WANAOCHUKUA MIKOP

                         SAME.                         

WAZIRI WA MADINI ANGELLAH KAIRUKI (WA TATU KUSHOTO) AKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA VIONGOZI NA WANACHAMA WA CHAMA CHA USHIRIKA WA AKIBA NA MIKOPO CHA WALIMU SAME SACCOS. 

WAZIRI wa Madini, Angellah Kairuki amewataka wananchi wanaokopa fedha katika taasisi mbalimbali kuwa makini na kusoma na kuelewa mikataba inayotolewa na taasisi hizo kabla ya kuchukua mkopo ili kuepuka kubebeshwa mzigo mkubwa wa riba.

Waziri Kairuki alitoa wito huo mwishoni mwa wiki katika mkutano mkuu wa 19 wa chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu Same Saccos iliyopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa, zipo baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikitoa mikopo kwa wananchi kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi badala yake zimekuwa zikiwakandamiza kupitia mikataba yao hali ambayo hupelekea mkopo kugeuka kama utumwa.

Waziri huyo alisema kuwa, Serikali ilipoasisi vyama vya kuweka na kukopa fedha ilikuwa na lengo la kuwakomboa Watanzania wote bila kusumbuliwa na kwa masharti madogo.

"Lengo la kukopeshwa kwa mwananchi ni ili kumuinua kiuchumi na sio kumkomoa kupitia mikataba migumu ambapo wananchi wengi wamekuwa hawapo makini katika kusoma mikataba na kuielewa vizuri na hatima yake ni kusumbuana katika marejesho" alisema Kairuki.

Waziri huyo aliwataka viongozi wa chama hicho cha Ushirika kuwa waaminifu na kuepuka kuwa na ubadhirifu wa fedha za chama ili kuwa na saccos iliyobora na kupelekea wanachama kujiunga kwa wingi.

Kairuki alisema hatua iliyochukuliwa na uongozi wa chama hicho kupunguza riba ya mkopo kwa asilimia 2 kutoka asilimia 18 hadi kufikia asilimia 16 ni jambo litakaloleta tija kwa walimu ambao ni wanachama kukopa mikopo kwa wingi na kuwataka viongozi hao kuona umuhimu wa kupunguza zaidi riba hiyo na kufikia asilimia 12 ili kuendana na ushindani na taasisi zingine za kifedha.

Aidha Waziri huyo aliwataka wanachama watakaokopa fedha kutambua kuwa fedha hizo zinatakiwa kurejeshwa kwa wakati na kuwataka kuepuka kukopa fedha na kuzifanyia shughuli zisizozalisha kwani itapelekea kuwa mzigo mkubwa katika marejesho.

Awali akisoma taarifa ya chama hicho, Mwenyekiti wa Bodi, Omari Mchome alisema kuwa, chama hicho chenye jumla ya wanachama 1533 inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ucheleweshwaji wa makato ya fedha za marejesho ya mkopo ya kila mwezi kutoka kwa mwajiri, wanachama kutotumia fursa ya kukopa saccos ipasavyo.


Mchome alisema kuwa, changamoto nyingine ni baadhi ya wanachama waliochukua mikopo kutorejesha mikopo hiyo kwa mujibu wa mkataba wa marejesho ulivyowekwa pamoja na baadhi ya wanachama kusimamishiwa mishahara kwa shida za utumishi.

"Wapi baadhi ya wanachama wanaasasi zaidi ya moja za kifedha zinazowahudumia na kushindwa kutumia fursa kikamilifu katika chama chao pia wapo baadhi ya wanachama wamehama wilaya na wengine kustaafu wakiwa bado wanadaiwa" alisema Mchome.

Mwisho

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ufahamu ugonjwa wa Ngiri ( Hernia) kiundani zaidi

Mama ajifungua mapacha wenye baba tofauti

UVCCM SIHA YAZINDUA KAMPENI YA KUGAWA TAULO ZA KIKE KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI